11 Novemba 2019 - 08:52
Rais Rouhani: Wananchi wa Iran wamesimama kidete pamoja mbele ya mashinikizo ya ajinabi

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kislamu ya Iran amesema kuwa, hii leo wananchi wa Iran wamejiandaa kuliko wakati wowote ule kwa ajili ya kujitolea na kutetea nchi hiyo.

(ABNA24.com) Rais Hassan Rouhani amesema hayo leo katika hadhara kubwa yenye hamasa ya wananchi wa Yazd (katikati mwa Iran) na kubainisha kwamba, Marekani inatambua vyema kuwa, wananchi wa Iran wamesimama kidete mbele ya mashinikizo yake dhidi ya taifa hili na si wenye kulegeza kamba.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, misimamo thabiti na isiyotetereka ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu imewakatisha tamaa maadui wa taifa hili pamoja na washirika wao

Rais Rouhani ameashiria takwimu za uchumi zinazoonyesha kuboreka uchumi wa taifa hili na kusema bayana kwamba, licha ya mashinikizo yote, lakini usafirishaji wa bidhaa za Iran zisizo za mafuta umeongezeka na hali ya uchumi wa taifa hili imekuwa ikiboreka kila mwezi ikilinganishwa na mwezi wa kabla yake.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza habari ya kuvumbuliwa medani mpya ya mafuta hapa nchini yenye hazina ya mapipa bilioni 53 ya mafuta na kueleza kwamba, katika mazingira ambayo maadui wamelenga na kuwekea vikwazo  uuzwaji wa mafuta ya Iran kwa ajili ya kuwashinikiza wananchi wa taifa hili, wataalamu na wahandisi wa Kiirani wamefanikiwa kuvumbua mapipa bilioni 53 ya mafuta katika sehemu moja yenye hazina kubwa ya mafuta.

Rais Rouhani amezungumzia kuanza leo maadhimisho ya Wiki ya Umoja na kubainisha kwamba, hii ni wiki ya kuonyesha umoja na mshikamano na watu kujikurubisha zaidi katika njia ya Bwana Mtume SAW.

..........
340